NGUVU YA MAAMUZI

SOMO: NGUVU YA MAAMUZI
MAANDIKO 2 WAFALME 7:3 – 15, MITHALI 23:7a

UTANGULIZI

MAAMUZI NI NINI?

MAAMUZI “ni chaguo analofanya mtu baada ya kufikilia jambo flani kulifanikisha"
Majadiriano/kusemezana kwa mtu aidha na nafsi yake ama watu wawili tofauti juu ya jambo fulani lenye utata ndicho mama/kiini wa Maamuzi, lakini Maamuzi ni matokeo ya ndani ya mawazo ya mtu/watu au Jawabu la mawazo ya mtu/watu. 2 FALME 7:3 “Basi walikuwepo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji wakasemezana, mbona tunakaa hapa mpaka tufe?
Tatizo moja kubwa sana ambalo huwa linachangia watu wengi wasiweze kufanikiwa katika maisha yao. Tatizo hili linaitwa kwa jina la hali ya KUSHINDWA/KUWA NA HOFU YA KUFANYA MAAMUZI KATIKA MAISHA.

Kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi watu wengi sana (hasa waliokoka/jamii ya waaminio) wamejikuta wakiwa katika hali zilezile bila kupiga hatua kwa muda mrefu sana katika maisha yao. Ukweli ni kuwa hali yako uliyonayo leo ni matokeo ya maamuzi ambayo uliyafanya huko nyuma, Hivyo kama hautaki kubakia pale ulipo leo ni lazima uamue kufanya aina ya maamuzi ambayo haujawahi kuyafanya kabisa katika maisha yako.

Yaone maamuzi ya wakoma wanne hawakutizama hali zao (udhaifu wao) wala hatari iliyokuwa mbele ya maamuzi yao bali kutimiza lengo la hitaji lao (chakula). Zaburi 72:13, 77:10.
Watu wengi wameshindwa kufanya baadhi ya maamuzi kwa hofu ya hali zao aidha kielimu, kiuchumi, familiya wanazotoka na nafasi zao. Zekaria 12:8, Yoeli 3:10c “aliye dhaifu na aseme mimi ni hodari”. (uhodari hubebwa na maamuzi, hakuna aitwaye hodari bila maamuzi Fulani juu ya jambo Fulani).
Kazi uliyonayo leo, biashara uliyonayo leo, maisha unayoishi leo ni matokeo ya maamuzi ambayo uliyafanya huko nyuma katika maisha yako. Hivyo basi kama ambavyo uliamua kuchagua maisha unayoishi sasa hivi, ndivyo ambavyo unaweza kuamua kuyabadilisha maisha unayoishi leo.
Hakuna mtu ambaye angeweza kubadirisha hali ya maisha ya wale wakoma wanne isipokuwa ni wao wenyewe kuamua kubaki katika lango la Samaria na wafe na njaa ama kufata jeshi la washami na wapate chakula kwao.
Kumbuka urithi wetu sisi tuliookoka uko ndani ya mikono ya wamataifa na Mungu amesema atawaamuru wataifa wakuletee urithi wako ni wewe tu kufanya MAAMUZI. Isaya 60:5, 11 “Malango yako nayo yatakuwa wazi daima, hayatafungwa mchana wala usiku, ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa, na wafalme wao wakiongozwa pamoja nao”.
Isaya 61:6 “Bali ninyi mtaitwa makuhani wa BWANA, watu watawaiteni wahudumu wa Mungu, mtakula utajiri wa mataifa na kujisifia utukufu wao”.
Hebu jichunguze katika maisha yako, kuna jambo ambalo hauridhiki nalo kabisa? Kuna kitu ambacho ungependa kibadilike? Kuna aina ya maisha ambayo unayapenda kuyaishi? Kama jibu lako ni ndiyo basi jua kuwa uwezo huo unao kama utakuwa tayari kufanya maamuzi bila uwoga wowote. Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi” (maamuzi), 2 Wafalme 7:4 “Haya! twende tukaliendee jeshi la washami”.
Watu ambao wamebakia katika hali zao bila kubadilika kabisa ni wale ambao kila wakati wanaishia kulalamika kuhusiana na aina ya maisha wanayoyaishi lakini hawako tayari kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na maisha yao, ni kama vile wanamsubiri mtu mahali fulani aweze kuwabadilishia maisha yao.
Kuna mambo katika maisha yako huwa yanaweza kubadilika kwa sababu muda umepita (kama ilivyo usiku lazima utaingia hata bila wewe kufanya maamuzi yoyote), lakini kuna mambo ambayo hayataweza kubadilika katika maisha yako hadi wewe mwenyewe uchukue hatua ya kufanya mabadiliko.
Kati ya vitu ambavyo ni lazima ufanyie maamuzi katika maisha yako ni kuamua kuwa hautakubali kushindwa katika maisha yako.
Ni lazima ifike hatua katika maisha yako ufanye maamuzi ya kufanikiwa; Mafanikio huwa hayaji kwa bahati katika maisha ya mtu, ni matokeo (mchakato) ya maamuzi ambayo mtu huyafanya. Kila unayemuona amefanikiwa katika maisha, jua kwamba kuna siku alifanya maamuzi ya kufanikiwa na hakukubali jambo (washami) lolote limkwamishe ama lifupishe safari yake. Je wewe umeshawahi kufanya maamuzi ya namna hii? Mara nyingi maamuzi haya hutakiwi kusubiri hadi uone dalili za mafanikio, unatakiwa kuyafanya wakati hata kukiwa hakuna dalili yoyote ya mafanikio. 2 Wafalme 7:5 “Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende
mpaka kituo cha Washami”. Hata kama leo maisha yako yanaoenekana kuwa hayana matumaini yoyote yale, hata kama inaonekana kama vile hautaweza kufikia lengo ulilojiwekea - Fanya jambo moja la muhimu leo: AMUA kuwa lazima utafanikiwa bila kujali chochote kile kitakachotokea katika maisha yako.
Ili kufanya maamuzi yatakayokusaidia katika maisha yako kuna hatua TATU unapaswa kuzichukua:
Moja ni ile hali ya kutambua na kukubali kwamba kuna uhitaji wa wewe kufanya maamuzi fulani. Watu wengi wanajikuta wamekwama mahali pamoja katika maisha yao kwa muda mrefu kwa sababu huwa hawataki kukubali kuwa wana matatizo. Kukataa tatizo hakufanyi tatizo kuondoka bali kunafanya ugumu wa kutatua tatizo uongezeke. Wengi ambao wamekata tamaa huamua kusema kuwa “mimi nimeridhika na maisha yangu au mimi nimeridhika na kazi yangu” lakini ukweli wa ndani ya moyo wao huwa wanatamani sana kubadilika na kuwa na maisha mazuri zaidi. MUSSA ninakwambia, Ili ufanye maamuzi yatakayoleta matokeo ni lazima ukubali kuwa una tatizo unalohitaji kulitatua. Hebu chunguza maisha yako leo, je kuna maeneo(Samaria) ambayo unahitaji kuyafanyia maamuzi.
Pili ni kutambua ni maamuzi gani unatakiwa kuyafanya. Kama umegundua kuwa kipato chako ni kidogo na matumizi yako ni makubwa, pengine utahitaji kufanya maamuzi ya kupunguza matumizi yako ama kuamua kutafuta kazi nyingine ya ziada. Mithali 10:4, 21:5
Kwa kila eneo la maisha yako ambalo umeona kuna uhitaji basi jitahidi kujiuliza hapa natakiwa kufanya uamuzi gani? -Mwingine itakuwa ni kutafuta kazi mpya, mwingine itakuwa ni kuvunja uhusiano na baadhi ya watu(wasio na mawazo chanya), mwingine ni kumwambia mtu ukweli badala ya kuendelea kuumia.
Hebu tafakari katika maeneo niliyotaja hapo juu ni maamuzi gani unapaswa kuyachukua?
Tatu ni kuchukua hatua ya kufanyia kazi maamuzi uliyoyaamua. Haitakusaidia chochote kama utaamua na kisha hautachukua hatua yoyote ile. Kuna watu wengi walishaamua kufanya biashara siku nyingi sana lakini hadi leo hawajaanza, kuna watu walishaamua kuanza upya maisha yao lakini kila siku wanarudi tena kwenye mahusiano ya zamani, kuna watu walishaamua kulima shamba lakini hadi leo hawana hata robo heka, wako mijini wanazurura tu, kuna watu kila ukikutana nao watakuambia kuwa wanataka kuwa wafugaji wa kuku lakini hata hawajaanza kufuga kuku mmoja n.k. Maamuzi bila hatua thabiti hayatakusaidia kabisa.
chochote ambacho umekifanyia mamuzi leo tafadhali chukua hatua na ukifanyie kazi bila kuchelewa. Na Mungu atakupa mpenyo na kukufanikisha kwa kishindo.
2 Wafalme 7:6 – 8 “Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu na mavazi, wakaenda wakavificha, wakarudi wakaingia katika hema ya pili vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha”.
Baada ya kusoma Somo hili hebu fanya MAAMUZI JUU YA HATMA YAKO
Kuna nguvu katika maamuzi, Mungu akubariki kwa viwango vya juu!!
Limeandaliwa na Mwl. Mussa Festo
Kwa mawasiliano na Ushauri: 0675415262
Email: mussafesto@gmail.com

Comments

Popular posts from this blog

JIFUNZE KUTII UPATE KUTIISHA