UMUHIMU WA KUJIJENGEA UWEZO ILI KULIBEBA KUSUDI LA MUNGU

 

KATIKA MAISHA YAKO. (CAPACITY BULDING).

 

NA MWL. MUSA FESTO

 

MAANDIKO YA MSINGI.

"Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele"(2Petro 3:18).

 

 " Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote"(Wagalatia 4:1)

 

MISINGI YA UUMBAJI.

 

Mungu alipokuwa anamuumba mwandamu na kumleta duniani kwa ajili ya kusudi lake kuna kiwango maalumu cha "kiutumishi"(kusudi na mapenzi makamilifu ya Mungu) ambacho Mungu alimpangia kila mmoja ili kwa kiwango hicho mwanadamu alitumikie kusudi la Mungu katika nyanja mbalimbali za kielimu,kiuongozi,kisiasa,kihuduma,kifamilia,kazi.n.k.

 

  "Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo"(Waefeso 2:10).

 

Tuone pamoja, anaposema "tutende metendo mema...... ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza tuenende nayo” ...sasa anapozungumzia tutende metendo mema. maana yake yapo mambo ambayo tunatakiwa kufanya, mahali pa kufanya na kiwango cha kuyafanya na kuyakamilisha hayo mambo katika kiwango ambacho Mungu alikusudia tokea awali yaani kabla ya kuumbwa kwa Misingi ya ulimwengu.

 

Daudi anasema.........

 

" Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado"(Zaburi 139:16).

 

Kitu gani nataka tutazame pamoja, ni hapo anaposema hayo maneno anamaanisha kuwa siku zake zote ambazo Mungu alikuwa amekusudia katika maisha ya Daudi yaani kazi, utumishi, mahali, kiwango cha utumishi kilikuwa kimeratibiwa kule juu mbinguni hata kabla Daudi hajafanywa katika mwili huu wa damu na nyama.

 

Bwana Yesu pia alizungumza maneno kama aliyosema Daudi pia......

 

"Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu"(Waebrania 10:7).

Kitu gani nataka tuone pamoja anaposema "katika gombo la chuo nimeandikwa”, maana yake ni kwamba Bwana Yesu anakiri ya kwamba maisha yake yote yameratibiwa katika gombo la chuo.

 

Sasa kwa mifano hiyo angalao kwa sehemu unaweza pata picha kwa sehemu ya kuwa kipo kiwango ambacho Mungu ameweka kwa kila mmoja ili aweze kukifikia anapotembea katika kusudi na mapenzi ya Mungu akiwa hapa duniani.

 

Sasa katika kulitimiza kusudi la Mungu duniani ipo sehemu ya Mungu katika kumsaidia mwanadamu ili aweze kulitumikia shauri la Bwana lakini ipo sehemu ya mwanadamu katika kushirikiana na Mungu ili kuweza kufikia katika kiwango ambacho Mungu alimuwekea kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.

 

Tunapoangalia sehemu ya Mwanadamu katika kushirikiana na Mungu ndipo tunazungumzia "umuhimu wa kujijengea uwezo binafsi ili kuweza kuibeba ndoto ya Mungu/Kusudi la Mungu katika maisha yako).

 

Unapozungumzia kwa habari ya kusudi la Mungu ni sababu ya kitu fulani kuwepo (The original intention of creation/making something). Mungu alipokuwa anamuumba mwanadamu kwa kusudi lake kuna vitu alimuumbia ndani yake kama vile vipaji, karama na huduma ili kwa hizo aweze kulitumikia kusudi la Mungu.

 

Lakini pia kuna vitu vingine alivifunga kwenye mazingira yanayomzunguka mwanadamu kama vile kiwango cha elimu, aina ya masomo, mahali pa kuishi, mahali pa kufanyia kazi n.k.

 

Hivyo vyote Mungu amevifunga kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu kufika mahali ambapo Mungu anataka aweze kufika.

 

Sasa sehemu kubwa ya mwanadamu ili kuweza kuyafanya hayo yote huku akishirikiana na Mungu ni kwa kujijengea uwezo ili kuweza kutembea katika kiwango ambacho Mungu amekikusudia kwa ajili yake kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.

 

" Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako"

(Isaya 54:2).

 

Yapo mambo kadhaa ambayo nataka tuangalie pamoja katika huo mstari angalau kwa sehemu.....

 

         Anaposema.... "panua mahali pa hema yako......”, maana yake ni kuwa kila mtu ana "hema”, ambamo ndani ya hema kuna vitu mbalimbali kama vile viti,watu,na mambo mengine mengine,kwa hiyo kwa maana nyingine hema ni kama kibebeo cha hayo mambo yote yaliyomo ndani.Sasa Mungu anampa mwanadamu ndoto katika mfumo wa picha inayojengeka ndani yake inayompa kusudi la kufanya jambo fulani.Kwa hiyo katika hilo neno Mungu anamaanisha kuwa ongeza uwezo wako wa kuibeba ndoto ya Mungu.

         Anaposema".....Ongeza urefu wa kamba zako",maana yake ni kwamba kamba inaunganisha sehemu moja na nyingine,kwa hiyo huyo mtu alikuwa anaenda kulingana na urefu wa kamba,kamba inapoishia ndiyo mwendo wako unaishia hapo.Sasa anaposema hilo jambo anamaanisha ya kuwa ongeza kiasi cha umbali wa ndoto uliyonayo.

         Anaposema ".....vikaze vigingi vya hema yako....",anamaanisha ya kuwa mhimili wa hema hiyo ni vigingi vinavyoshikilia hilo hema (Nguzo),kwa maana rahisi hapo anamaanisha kujenga msuli wa ndani utakaokusaidia kuibeba hiyo hema(Ndoto ya Mungu) kwa kujenga mahusiano mazuri na mtoa ndoto,yaani Mungu,yeye anayeweza kuimarisha misuli yako na kushiriki katika kukujengea uwezo huo kwani .... "Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure"(Zaburi 127:1a).

 

Ni nia na makusudi kabisa ya Mungu kuona watoto wake wakijijengea uwezo binafsi kwa kushirikiana na Mungu ili kuibeba ndoto ya Mungu.

 

Kwa kadri unavyozidi kujijengea uwezo binafsi wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako ndivyo ambavyo Mungu atakupa hatua zaidi.

 

 

TUJIFUNZE KUTOKA KWA HAWA NDUGU KATIKA IMANI.

 

Mfano wa kwanza.

Mungu alipokuwa anamwita Abrahamu. (Mwanzo 13:14-15).

 

Tunaposoma kwa habari za Baba yetu katika imani (Abraham) Mungu alipomwita na kumwambia na kumilikisha baraka kwa ajili yake na uzao wake alimwambia maneno yafuatayo......

 " Bwana akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele"

(Mwanzo 13:14-15).

 

Kuna mambo nataka tuyatazame pamoja katika mistari hapo juu...

 

I).Unapotaka kujijengea uwezo katika jambo fulani ni lazima uwe na mtazamo thabiti juu ya hilo jambo (to have a focus) .Kwa hiyo kuna watu,marafiki na vitu vingine ambavyo kwako ni muhimu sana lakini katika hilo jambo unalotaka kujijengea uwezo havitakufaa ni lazima ukubali gharama ya kuviacha ili kujijengea uwezo katika eneo sahihi.Mungu alimwambia Abram alipokuwa anamtoa Uru ya wakaldayo kuwa awaache hata ndugu zake lakini yeye aliondoka na Rutu (Mwanzo 12:1-5,Mwanzo 11:7).Baada ya Abramu kuachana na Rutu ndipo Mungu akazungumza naye (Your association will determine your destination).

 

II).Suala la kujijengea uwezo ni suala la maelekezo na maagizo na Ruhusa ya Mungu kwa mwanadamu.Hakuna mwanadamu ambaye anaweza akajijengea uwezo pasipo kumshirikisha Mungu kwa sababu yeye ndiye aliyemuumba mwanadamu kwa hiyo anajua alimuumba kwa kazi gani kwa hiyo hata katika eneo la kujijengea uwezo ni suala la Mungu zaidi......."inua sasa macho yako ukatazame kutoka hapo ulipo...."

 

 

 " Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure"(Zaburi 127:1).

 III). Japokuwa suala la kujijengea uwezo binafsi linamhitaji Mungu zaidi kuwa kama kitovu (center) linahitaji pia utayari wa mwanadamu katika kushirikiana na Mungu ili aweze kujijengea uwezo katika eneo husika. Mungu alivyomwambia Abram inua sasa macho yako ukatizame...uamuzi wa kuinua au kutokuinua...kutizama au kutokutizama ulikuwa mikononi mwa Abram.Mungu haitaji mtu aliyekamilika hata siku moja,anamhitaji mtu aliye tayari,ili amkamilishe katika neema yake na ukamilifu wake.....

 

III).Mungu alimwambia Abramu atizame pande zote mpaka pale upeo wa macho yake utakapofikia,na ule ukubwa wa nchi auonao kulingana na upeo wa macho yake Mungu atampa aimiliki,hii inamaanisha ya kuwa katika ile nchi ni lazima kulikuwa na milima,mabonde ,mito na mambo Mengine mengi ambayo yangemfanya Abram asione mbele zaidi,lakini Mungu alimwambia kitu cha ajabu sana kuwa........maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele",hii inamaanisha ya kuwa  "kiwango cha upeo wa macho yake kuona utakapoishia ndipo kiwango cha urithi wake na uzao wake utakapoishia",sasa hapa suala la Abramu kujijengea uwezo binafsi wa kujenga kuona zaidi ile nchi kwa kukabiliana na milima,mito,mabaonde na mambo yanayofanana na hayo ulikuwa ni wa muhimu sana kwake.Mungu asingeweza kumpa urithi zaidi ya pale mahali upeo wa macho yake umeishia.

 

 

Mfano wa Pili.

Watumwa waliopewa talanta.

 

Jambo la kwanza: Mungu anakupa kitu kulingana na uwezo ulionao.

 

" Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri". (Mathayo 25:14-15).

 

Kitu gani nataka tutizame pamoja katika mstari huo ni kwamba Mungu alitoa talanta kwa kila mmoja kulingana na uwezo alionao wa kuibeba hiyo talanta, kwa hiyo hakuna namna Mungu anavyoweza kukupa kitu chochote kama hauna uwezo wa kukibeba kitu hicho.

 

Jambo la pili: Kwa kadri unavyoongeza uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako ndivyo Mungu anazidi kuipanua hema yako na kukuongeza.

 

 "Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.

 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.  Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.  Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.  Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.  Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.  Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

(Mathayo 25:19-28).

 

Tunaposoma habari hiyo tunaona namna ambavyo wale watumwa ambao walipewa talanta tano na mwingine mbili waliweza kuzalisha mara mbili zaidi na hivyo wakawa wameongeza uwezo wao wa kubeba kile kitu Mungu kawapa na kumzalia Mungu matunda, lakini yule mmoja ambaye Mungu alimpa talanta moja kwa kadri ya uwezo alionao hakuweza kumzalia Mungu matunda akanyanganywa ile talanta ambayo Mungu alimpa na akapewa mtu mwingine aliyekuwa amejijengea uwezo wa ndani wa kuibeba ndoto ya Mungu.

Inawezekana kabisa kujijengea uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu, haijalishi mazingira uliyonayo lakini inawezekana, hao ndugu wote walikuwa ni watumwa ambao wamepewa talanta, sasa unaweza ukaelewa, mtumwa muda si mali yake na siku zote hana uhuru wa kufanya kazi kama mtu aliye huru, lakini kwa nini hao watu wanaoishi katika mazingira yanayofanana karibu kwa kila kitu mmoja afanikiwe kuzalisha zaidi na mwingine hata akashindwa???... ukiamua inawezekana.

" Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa"(Mathayo 25:19).

 

Mfano wa tatu.

Bwana Yesu alipokuwa akiwaaga wanafunzi wake. (Yohana 16:12).

 

Tunaposoma habari za Bwana Yesu namna alivyokaa na wanafunzi siku zote alipokuwa akitembea katika kulibeba kusudi la Mungu, Bwana Yesu alikuwa akijitahidi kuwajengea "uwezo binafsi" kila mmoja, ndiyo maana alikuwa akiwasisitiza sana kwa habari ya swala la Maombi.

 

Lakini alipokuwa akiondoka kuna kitu cha ajabu sana aliwaambia......

 

  "Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa"

(Yohana 16:12).

 

Kitu gani Yesu kilimzuia kuzungumza na hao wanafunzi wakati anaondoka ni kwamba walikuwa hawana uwezo wa kuyabeba hayo mambo, alikuwa anazungumza juu ya kujijengea uwezo binafsi ili waweze kukibeba kile kitu Yesu atawaamba. Ndiyo maana Yesu anasema kuwa anakupa kitu kulingana na uwezo ulionao kukibeba. Kwa kadri unavyoendelea kujijengea uwezo katika eneo husika ndivyo Mungu anazidi kuachilia maono na ndoto zake kwako.

 

Mfano wa nne.

Wana wa Israeli wakiwa katika nchi ya ahadi.

 

Tunaposoma kwa habari za wana wa Israeli tunaona ya kuwa Mungu aliwapa nchi ya Kaanani yenye maziwa na asali ili waimiliki.

 

"Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao". (Kutoka 13:1-2).

 

Kitu gani nataka tuone pamoja mahali hapo, ni hayo maneno ambayo nimeyapigia mstari, Mungu aliwapa wana wa Israeli hiyo nchi kwa sababu alijua ya kuwa wanao uwezo wa kuimiliki.

 

Lakini kuna kitu nataka tuone pamoja mahali hapo, ile nchi ilikuwa inakaliwa na majitu yenye nguvu kiasi cha kwamba hata wale wapelelezi wengine walipokwenda walijifananisha kama mapanzi. (Kutoka 13:31-33).

 

Japokuwa ni Mungu aliwapa hiyo nchi kwa kujua kabisa wanao uwezo wa kuimiliki hiyo nchi, Mungu aliwaambia kitu cha ajbu sana wana wa Israeli.

 

" Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi"(Kutoka 23:29-30).

 

Kwa maneno hayo niliyoyapigia mstari, Mungu alikuwa anamaanisha kuwa uwezo wao wa kuimiliki nchi utakapoongezeka, ndivyo ambavyo Mungu atawafukuza maadui katika ile nchi aliyowaahidi na kuwapa wana wa Israeli. (Capacity bulding).

 

Mfano wa tano.

Musa katika kuwahukumu watu (kutoka 18).

 

Ilikuwa ni baada ya Mungu kuwatoa kutoka Misri na kuingia katika nchi ya ahadi ambayo Mungu amewapa, huduma ya Musa sasa ikachanua, idadi ya watu aliokuwa anawahudumia ikawa kubwa sana kiasi ambacho Ilimbidi Musa awe anawahukumu watu hao kuanzia asubuhi hata jioni

(kutoka 18:13-14).

 

Mungu alimtumia mkwewe Musa yaani mzee Yethro kuzungumza na Musa maagizo haya.....

 

".... Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao"

(kutoka 18:19).

 

 ".......Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe”. (Kutoka 18:21-22).

Kitu gani nataka tujifunze mahali hapo ni kuwa Mungu alizungumza na Musa kwa kumtumia mzee Yethro kuwa achague watu wenye uwezo ambao kila mtu atasimsmia kundi la maelfu, mia hamsini na kumi kulingana na uwezo alionao. Kwa hiyo hii inatujulisha kuwa Mungu anatoa kitu kulingana na uwezo ulionao. Inawezekana ndani yako kuna ndoto ya kuwa kiongozi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kihuduma n.k. Ni muhimu sana kuendele akujijengea uwezo ili uweze kuibeba hiyo ndoto.

 

 

 

 

 

Mfano wa sita.

Daudi alipokuwa anamkabili Goliath (1samweli 17:34-37).

Ndoto ya Mungu juu ya Daudi ilikuwa ni kumtumia Daudi ili kumuua Goliathi. Lakini Mungu hakumkutanisha Daudi moja kwa moja na Goliathi, nilimbidi Mungu ampitishe kwanza Daudi kwenye mazoezi madogomadogo akiwa machungani ili "kumjengea uwezo" kabla hajakutana na Goliath.......

Daudi akieleza namna alivyojijengea uwezo akiwa machungani....

 "Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua, Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai."(1Samweli 17:34-36).

 

Hapo Daudi alikuwa akitaja wasifu wake (CV) mbele za mfalme sauli, alichokuwa anaeleza hapo ni uwezo alionao, na kitu gani Sauli alikuwa anatafuta kwa Daudi ni "kujua uwezo alionao" wa kupambana na Goliath.

Alipokuwa akikabiliana na Goliath alisema maneno haya...........

 "Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe"(1Samweli 17:37).

 

Mfano wa saba.

Daudi alipokuwa anapewa nafasi kuwa mfalme wa Israeli. (1Samweli 1:1-3).

Ndoto ya Mungu kwa Daudi ilikuwa ni kumtoa Daudi katika hali ya chini sana na kumweka kuwa mfalme wa taifa la Israeli badala ya Sauli.

 " Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe"(1Samweli 16:1).

 

 "Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama"(1Samweli 16:13).

 

Lakini pamoja na kwamba Mungu alikuwa amemkusudia Daudi kuwa mfalme wa Israeli yenye jumla ya kabila kumi na mbili, Mungu alimchukua Daudi hatua kwa hatua......

 

Hatua ya kwanza. (2Samweli 2:4).

 "Basi watu wa Yuda wakaenda, wakamtia Daudi mafuta huko, awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Wakamwambia Daudi wakasema, Watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Sauli"(2Samweli 2:4).

 

Ndoto ya Mungu juu ya Daudi ilikuwa ni kuwa mfalme wa taifa la Israeli lenye jumla ya kabila kumi na mbili, lakini kwa mara ya kwanza Mungu alimpa Daudi kuwa kiongozi wa kabila la Yuda.

 

Kumbuka kuwa ndani ya Daudi Mungu alikuwa ameweka ndoto na nguvu (upako) wa kuwa mfalme juu ya Taifa la Israeli kama tulivyokwisha kuona hapo juu. (1Samweli 16:13).

 

Daudi alikaa hapo akijenga uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu kwa miaka saba na miezi sita....

 

 "Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita"(2Samweli 5:5a).

 

 

Hatua ya pili (2Samweli 5:3).

 

Baada ya Daudi kuwa mwaminifu kuliongoza kabila moja (Yuda) na kujenga uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu ndipo Mungu akampa taifa zima la Israeli lenye kabila kumi na mbili..........

 

 " Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda"(2Samweli 5:3-5).

 

Ilikuwa ni lazima Daudi aweze kujijengea uwezo binafsi ili aweze kuibeba ndoto ya Mungu kuwa mfalme wa Israeli, kumbuka baada ya kuwa mfalme wa Israeli mji wake mkuu ulikuwa ni Yerusalemu iliyokuwa inatawaliwa na Wayebusi ambao walikuwa ni watu mashujaa, ilikuwa ni lazima Daudi awaondoe Wayebusi ili aweze kutawala nchi hiyo, na ndiyo maana Kabla ya kukutana na Yebusi Mungu alimpitisha kuwa Mfalme wa Yuda ili ajijengee uwezo wa kuikabili hiyo changamoto.

 

 " Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo.  Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi"(2Samweli 5:6-7).

 

Mfano wa saba: Waebrania

 

"Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. (13) Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. (14) Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya"(Waebrania 5:12-14).

 

MAMBO YA MSINGI YATAKAYOKUSAIDIA KUJIJENGEA UWEZO BINAFSI ILI KULIBEBA KUSUDI LA MUNGU KATIKA MAISHA YAKO.

 

i). TAFUTA KULIJUA KUSUDI LA MUNGU KATIKA MAISHA YAKO.

 

Hii ni Hatua ya kwanza na ya msingi kabisa katika kujijengea uwezo binafsi wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako.

 

          Kusudi linakupa kujua sababu ya kuumbwa kwako, (The reason for creation). Ulimwengu huu tunaoishi una mambo mengi ya kila namna ambayo yanaweza kutumika kama upepo kukuyumbisha huku na kule na hivyo ukashindwa kuwa na mwelekeo thabiti juu ya maisha yako. Kulijua kusudi la Mungu itakusaidia kupanga mipango, kuwekeza nguvu, muda, fedha na kuweka vipaumbele kwa kuangalia kusud, yaani unaishi maisha yanayoongozwa na kusudi "Purpose driven life".

 

           "Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama"(Mithali 19:21).

 

 

          Mungu huweka Maono, ndoto na matamanio ndani ya mtu kulingana na kusudi ambalo amemuumbia. Kusudi la Mungu limewekwa katika namna ya picha ndani ya mtu inayoonesha kukamilisha jambo fulani au mwisho wa jambo fulani. Mungu anaweza weka ndani yako ndani yako ndoto ya kuwa kiongozi katika nyanja ya siasa, huduma, uimbaji.n. k Ni muhimu sana ya kuanza kujenga uwezo katika maeneo hayo.

 

 " nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo                          yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote"(Isaya 46:10).

 

          Ipo neema ya kukua unaposimama katika kusudi na mpango wa Mungu.Mungu alituumba wanadamu tofauti tofauti na aliiweka neema ya kukua kwa kila mmoja katika eneo lake. Kama wewe Mungu alikuumbia kuwa mwalimu. itakuwa ni vigumu sana kukua katika uinjilisti, kama alikuumbia kuwa daktari itakuwa vigumu sana kukua katika engineering.

 

          "Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele"(2Wakorintho 3:18).

 

           "Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye"

(1Wakorintho 3:7).

 

ii). UHUSIANO WAKO BINAFSI NA MUNGU.

Uhusiano wako binafsi na Mungu ni jambo la Msingi sana katika kujijengea uwezo binafsi wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako. Itakuwa ni vigumu sana kulijua kusudi la Mungu katika maisha yako kama hauna mahusiano binafsi na Mungu, kumbuka kwamba Mungu aliyekuumba anajua kuwa alikuumba kwa kazi gani, kwa hiyo ukitaka kujua kazi yako hapa duniani ni lazima uende kwake yeye aliyekutengeneza (The manufacturer know the purpose of the products).

Swala la mahusiano binafsi na Mungu sio swala la kufuata mkumbo au kundi, kumbuka nimesema kuwa "mahusiano binafsi" kiasi ambacho Mungu anazungumza na kuhusika kikamilifu katika hatua za maisha yako.

 

Unapozungumzia swala la kujijengea uwezo binafsi wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako uwe na uhakika kuwa Mungu mwenyewe anahusika kikamilifu katika kukujengea huo uwezo kwa sababu yeye ndiye muumba wako, anajua unatakiwa ubebe kitu gani, na anajua hicho kitu unachotakiwa kukibeba kinahitaji nguvu kiasi gani na anajua ya kuwa unatakiwa kwenda umbali kiasi gani na hiyo ndoto, na tena anajua ifanyike kwa ustadi kiwango gani.

 

Usije ukafanya kosa la kujijengea uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako huku ukimwacha yeye anayeijua ndoto yake juu yako pembeni. Kumbuka hili ya kuwa uhusiano wako na Mungu ni wa Muhimu sana kuliko utumishi wako mbele za Mungu (Your relationship with God is more important than your mission for God).

 

 " Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure"(Zaburi 127:1).

 

 

 

III). KUWA NA TAARIFA SAHIHI.

 

Kuwa na taarifa sahihi juu ya ndoto uliyonayo ni jambo la muhimu sana. Kuwa na taarifa kunakusaidia kujua kwa undani hilo jambo kiasi ambacho unakuwa na nguvu ya kukusaidia kulimiliki au kulitawala eneo hilo. (Information is power).

 

Hili ni jambo ambalo hata tunaliona katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kielimu, kihuduma, kiuchumi na hata kiutamadumi, watu waliofanikiwa ni wale walio na taarifa sahihi kulingana na maeneo hayo. Jitahidi kujijengea tabia ya kupata taarifa sahihi kutoka kwa watu, nyaraka mbalimbali zilizotunzwa kwa njia ya Vitabu, majarida hata sauti kwa njia ya Sauti. Hili jambo lilimsaidia hata Danieli kujua ya kuwa Muda wao wa kukaa utumwani ulikuwa umekwisha.....

 

 " katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini"(Danieli 9:2)

Danieli alipata taarifa kwa kuvisoma vitabu, alisoma vitabu gani (2Nyakati 36:21, Yeremia 25:11-12, yeremia 29:10)

 

IV). NGUVU YA MAOMBI.

 

Unapozungumzia nguvu ya maombi ni jambo la msingi sana pia katika kujijengea uwezo binafsi wa kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako katika eneo ambalo Mungu amekupa.Kwa njia ya maombi Mungu anazidi kuachilia maono katika hilo jambo,lakini pia Mungu anatumia njia ya Maombi ili kukujengea "msuli wa ndani" utakaokusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali unapotembea katika ndoto hiyo.Shetani asingetaka ujenge uwezo katika hilo jambo ambalo Mungu amekupa kulifanya kwa hiyo kwa njia ya maombi unaweza kuziangusha ngome na kila fikra zinazojiinua kinyume na mpango wa Mungu juu ya maisha yako.

Hebu Tuangalie mifano hii michache.

Mfano wa kwanza.

Nehemia katika kuujenga ukuta wa Yerusalemu na malango yake yaliyochomwa.

Unaposoma kitabu chote cha Nehemia tunaona ya kuwa kusudi la Mungu juu ya Nehemia ilikuwa ni kwenda kuujenga ukuta wa Yerusalamu pamoja na malango yake yaliyochomwa moto. Hii haikuwa kazi Rahisi kwa sababu walikutana na upinzani mkubwa sana dhidi ya Sanballat na Tobia. Lakini kilichomsaidia Nehemia ni kwamba alikuwa ana nguvu ya maombi aliyoanza nayo kabla ya kuingia kazini.

"......Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni"(Nehemia 1:3-4).

 

 

 

 



Nehemia akikutana na upinzani Dhidi ya akina sanballat.....

 

 " Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo"(Nehemia 4:7-8).

 

 

Kwa sababu ndani yake Nehemia alikuwa amejijengea uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo kwa njia ya maombi aliyoanza nayo mwanzoni hakuiacha ndoto ya Mungu njiani, aliibeba mpaka pale alipomaliza.

 

  "Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili"(Nehemia 6:15).

 

Mfano wa pili.

Yesu alipokuwa Gethsemani akiomba kuelekea msalabani.

 

Ndoto ya Mungu juu ya Bwana Yesu ilikuwa ni Yesu kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Lakini haikuwa kitu rahisi kwa Bwana Yesu kuibeba ile ndoto pale alipokuwa akikaribia kwenda msalabani, aliingia kwenye maombi mazito kiasi cha jasho misiri ya damu kumtoka, alipokuwa anakaribia kwenda msalabani (kuibeba ndoto ya Mungu) alisema maneno haya ya kusema....

 

 " Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe"(Mathayo 26:39).

 

 " Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe"(Mathayo 26:42).

 

 

"Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale"

(Mathayo 26:44).

Tunaposoma maneno hayo tunaona namna ambavyo Yesu alikuwa amekosa ujasiri wa kulibeba kusudi la Mungu yaani kuelekea msalabani. Lakini aliendelea kumwomba Mungu mahali pale na kupitia maombi yale Mungu alikuwa akimtengenezea msuli wa ndani ili aweze kuibeba ndoto ya Mungu, na katikati ya maombi yale Malaika akaja na kumtia nguvu (Kumwongezea uwezo wa kuibeba ndoto ya Mungu) ...

 

"Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.  Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini"(Luka 22:43-44).

Je ni mara ngapi huwa unaingia katika maombi na kumwomba Mungu kwa habari ya ndoto ambazo ameweka katika maisha yako, je unao ujasiri wa kutosha wa kuiendea hiyo ndoto na kuifanya kuwa kiti dhahiri, jitahidi kukaa katika maombi kwa muda wa kutosha ilim kujijengea misuli zaidi na ujasiri wa kuibeba hiyo ndoto kwa utukufu wa Mungu.

 

 

V) NGUVU YA UVUMILIVU. (The power of perserverence).

Katika swala zima la kujijengea uwezo binafsi kwa ajili ya kuibeba ndoto ya Mungu katika maisha yako uvumilivu ni jambo la msingi sana. Unapokuwa katika hizo hatua kuna mambo mengine utakayokutana nayo na itatakiwa kukabiliana nayo, vipingamizi, vikwazo, kuchukuliana na watu na hata wakati mwingine unaweza kuanguka (ups and downs), lakini jambo la msingi ni kuwa mvumilivu.

 

 "Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu"(Mika 7:8).

 

 " Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake.  Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza"(Zaburi 37:23-24).

 

Kitu gani nataka tuone pamoja kwenye hiyo mistari ni kuwa katika safari yoyote ya kuelekea kwenye ndoto yako kuna kuanguka lakini hii isikukatishe tamaa kama mika anavyosema hapo juu kuwa "niangukapo nitasimama tena”, lakini pia wakati mwingine unaweza kujikwaa katika baadhi ya mambo uwe na uhakika ya kuwa Mungu atakusimamia na kukupigania mpaka pale ndoto hiyo itakaposimama kama Muimba Zaburi anavyosema kuwa "Bwana humshika mkono na kumtegemeza"

 

Swala la kujijengea uwezo ni mchakato (Process) na si jambo la siku moja tu (an overnight process), hivyo linahitaji kujitoa kikamilifu kabisa, Mungu atakuchukua hatua kwa hatua ili kuiendea ile ndoto aliyoiweka katika maisha yako. Mungu anafanya kila jambo kwa wakati maalumu kwa hiyo hata anapokupitisha darasani kwa ajili ya kukujengea uwezo huo anajua unahitaji kukaa katika hilo darasa kwa muda gani.

 

Mungu alimwambia Habakuki maneno haya...

"Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia"(Waebrania 2:3).

 

Kwa maneno hayo Mungu alikuwa akizungumza na Habakuki kwa habari ya kuwa mvumilivu kusubiri kwa maana ile ndoto ni kwa wakati ulioamriwa.

 

MAENEO MUHIMU/AINA YA UWEZO UNAOWEZA KUJIJENGEA

v  Uwezo wa Kuitambua ,kuisikia sauti ya Mungu…kwa bidii

v  Uwezo wa kukiatamia kile kitu Mungu ameweka katika maisha yako (Kuliatamia yai ambalo Mungu ameweka kwenye maisha yako ili utotoe kifaranga-an ability to incubate)

v  Uwezo wa kubadili mfumo wako mzima wa kufikiri (Gods plan versus your plan….Yeremia, Gideoni)-Ability to remove the inferiority complex

v  Ability to resist bad news……. Taarifa gani unaisikia na ni kwa wapelelezi gani??

v  Uwezo wa kufanya kazi kama team

v  Uwezo wa kuwachukulia watu na madhaifu waliyonayo…Eg. Jesus versus petro

v  Uwezo wa ku-Master eneo ambalo Mungu anataka umtumikie

v  Uwezo wa ku-handle failure

v  Uwezo wa ku-handle success

v  Uwezo wa kuvumilia na kuzitazamia ahadi za Mungu

v  Uwezo wa kutunza siri mbalimbali za Mungu

v  Uwezo wa kuwa na utulivu wa Rohoni na kuisubiri saa ya Bwana

v  Uwezo wa kuwa na ufahamu juu ya majira na nyakati na kujua mambo ya msingi unatakiwa kufanya kwa kuzingatia majira na nyakati hizo.

 

 

Nakutakia mafanikio mema pindi unapoendelea kujijengea uwezo wa kulibeba kusudi la Mungu katika maisha yako, niseme tu kwamba Mungu analokusudi kubwa sana juu ya hiyo ndoto aliyoiweka katika maisha yako, wako watu wengi sana huku wanasubiri kuvuka mahali waliko kwa kufanikiwa kwako wewe katika ndoto hiyo/kusudi hilo, yaani ndoto hiyo imebeba pia maisha ya watu wengine, jifunge mkanda, simama kikamilifu. mlingane Mungu na uudhihirishie ulimwengu thamani ya ile ndoto Mungu ameiweka katika maisha yako kwa utukufu wa Mungu. Inawezwekana kwa yeyote aliye tayari kulipa gharama ili kuifanikisha.

Japokuwa kuna ghrama katika kujijengea uwezo na kuibeba kusudi la Mungu, lakini ipo neema ya kumsaidia kila mmoja katika eneo lake. 

 

Wako katika kuujenga Mwili wa KRISTO(Kanisa)

Mwl.Musa Festo

Mungu akubariki kwa viwango vya juu.

Contacts: 0675415262.

mussafesto@gmail.com.

 

Comments

Popular posts from this blog

JIFUNZE KUTII UPATE KUTIISHA